Friday, 16 June 2017

Mkutano wa wadau wa iCHF - Kilimanjaro


Wenyeviti wa Halmashauri za Kilimanjaro, Wakurugenzi wa halmashauri na wadau wengine wakihudhuria mkutano wa nusu mwaka wa wadau wa iCHF

Monday, 29 May 2017

Mwanga na Same, tumewafikia......


Kaimu Mkurugenzi halmashauri ya same (Juu) akijaribu pikipiki kabla hajaikabidhi kwa waratibu wa CHF iliyoboreshwa wa tarafa. Chini, Mkurugenzi wa halmashauri ya Mwanga akimkabidhi pikipiki mmoja ya mratibu wa tarafa tayari kwa kuanza kazi ya usajili CHF iliyoboreshwa

Sunday, 26 March 2017

Wanakijiji wanavyofaidika na CHF iliyoboreshwa

Wanakijiji wametoa ushuhuda juu ya kufaidika kwao na Mfuko wa Afya ya Jamii ulioboreshwa (iCHF).

Wanakijiji hao wa Singa, Kata ya Kibosho Mashariki, Tarafa ya Kibosho, Wilaya ya Moshi Vijijini wameelezea kufurahishwa na kupatiwa huduma za afya zenye kiwango cha juu bila usumbufu, tena kwa gharama nafuu.

Wilaya ya Moshi Vijijini ni miongoni mwa wilaya za Mkoa wa Kilimanjaro na Manyara zinazopata huduma ya iCHF. Nyingine mkoani Kilimanjaro ni Siha, Hai, Rombo, Mwanga na Same.

Mmoja wa wafaidika hao, Bw Faustine Leruba anasema kwamba CHF iliyoboreshwa imemsaidia sana na mke wake, kwa sababu sasa kila akihisi kuumwa huenda hospitalini na kupata matibabu na kwamba kwenye hii iliyoboreshwa hakuna usumbufu, na dawa hupatikana vizuri. Amekuwa akipata matibabu katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Kibosho.

Bw Leruba (72) alijiunga na iCHF Februari mwaka jana (2016) baada ya Wasamaria wema kumsaidia fedha kwa ajili hiyo, ambapo amejiunga pamoja na mkewe. Anasema kwa kujiunga huko, kwa kulipia 30,000/- kwa mwaka kunawapunguzia sana gharama kubwa za matibabu. Anakiri kwamba hakuwa akiujua mpango huo hadi aliposikia ukitangazwa kwenye Ibada ya Misa Jumapili katika Kanisa Katoliki Kibosho, karibu kabisa na Kibosho Hospitali.

Hata hivyo, Leruba anasema kwamba hakuweza kujiunga kwani aliona kwamba hakuwa na fedha, japokuwa akiugua angefanya kila awezalo kupata fedha kwa ajili ya matibabu na wakati mwingine angekopa kwa marafiki au majirani. Anasema kwamba kwa wastani kila akienda hospitali kwa ajili ya matibabu aliingia gharama ya zaidi ya 10,000/-.

Akifafanua zaidi juu ya hali hiyo, anasema ukokotozi unaonesha kwamba malipo yaliyofanywa na familia yake kwa ajili ya matibabu kwa mwaka ni zaidi ya 300,000/- ikiwa hawatumii iCHF, kwani huenda hospitali mara kwa mara kwa sababu ana matatizo ya miguu – gauti.
Anasema kwamba mbali ya yeye kuugua na kuhitaji matibabu mara kwa mara, mkewe pia ana matatizo makubwa ya kifua, hivyo hutakiwa kwenda hospitali mara kwa mara kwa ajili ya uangalizi na matibabu. Anasema laiti wasingekuwa na CHF iliyoboreshwa, basi wangedidimia zaidi kwenye umasikini. Bw Leruba alikuwa muuza duka jijini Dar es Salaam kwa miaka mingi kabla ya kuamua kurejea kijijini baada ya maisha kumpiga kwenye jiji hilo kuu kibiashara. Mkewe ni mfanyabiashara, anayetengeneza na kuuza pombe ya mbege kwa jumla.

iCHF sasa inatekelezwa na mabaraza ya halmashauri za wilaya chini ya ulezi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF). Shirika lisilo la kiserikali – PharmAccess hutoa usaidizi wa kiufundi kwa ajili ya utawala na kuboresha huduma za afya pamoja na shughuli za masoko kwa ajili ya iCHF.

Ili kuboresha kiwango cha huduma za afya, zahanati, vituo vya afya na hospitali za umma na binafsi zilizo kwenye iCHF zimeingizwa kwenye program ya SafeCare. NHIF na PharmAccess kwa pamoja huwezesha uboreshaji wa miundombinu kwenye huduma zinakotolewa, kwa kuvutia uwekezaji, kuhakikisha huduma bora zinatolewa na mpango huu na kijiografia kuongeza maeneo yanayopatiwa huduma.

Mlengwa mwingine ni Bw Dionis Neneu (67), kutoka kijiji hicho hicho, anayesema kwamba anafurahia huduma ya kiwango kizuri ya afya bila kuingia kwenye tabu ya kutafuta fedha kila mara kwa ajili ya kugharamia, huku akiwa hajui ingegharimu kiasi gani cha fedha.

Bw Neneu anasema kwamba alihuisha huduma hiyo ya CHF iliyoboreshwa Januari mwaka huu, kwani kwa mara ya kwanza alikatiwa na mtoto wake mwaka jana, ambapo iCHF hiyo inamhusu yeye na mkewe.

Wanafurahia maisha kwa sabbau katika umri wao mkubwa wanapata huduma ya afya kila wakati wanapoihitaji. Wote wawili ni wakulima ambao pia hufuga ng’ombe nyumbani kwao.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Singa, Bw Paul Lazaro anasema pamekuwa na mwamko mkubwa wa watu wanaojitokeza kwa ajili ya kujiunga iCHF. Hali hiyo, anasema, inatokana na watu kuongezewa uelewa juu ya umuhimu wa kuwa na bima, kazi ambayo imekuwa ikifanywa na maofisa au wadau wa NHIF kwenye nyumba za ibada na viongozi wa kisiasa kwenye mikutano mtawalia.

Chini ya mpango huo, kaya inaweza kuorodhesha hadi wana familia sita hivyo kuwa na haki ya kupatiwa huduma za matibabu n ahata kulazwa hata kwa magonjwa makubwa, huduma ya msingi ya meno pamoja na upasuaji wa dharura, ukihusisha pia wakati wa uzazi. Serikali, kupitia NHIF, hujazia asilimia 50 ya gharama kwa kundi husika.


Ile hali ya kufanya wananchi wamiliki mpango wenyewe, huku kukiwapo na kujengewa uwezo kutoka kwa PharmAccess, husaidia na kuhakikisha kwamba unakuwa mradi endelevu.

Saturday, 4 March 2017

Uandikishaji wa wanachama wa iCHF unatumia vifaa vya kielektroniki, hauna haja ya kuingia gharama kupiga picha. Waandikishaji watakupiga picha wewe pamoja na familiai yako

Friday, 3 March 2017

Uboreshaji wa huduma unaofanywa na iCHF

Ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora, iCHF imekuwa ikisaidia uboreshaji wa huduma kwenye zahanati na vituo vya afya wilayani.

Madiwani Mwanga, Same wapitisha CHF iliyoboreshwa kuanza wilayani kwao!

Waheshimiwa madiwani wa halmashauri ya Mwanga wakimsikiliza meneja wa mkoa wa Kilimanjaro wakati wa semina kwa madiwani kuhusu CHF iliyoboreshwa.

Thursday, 2 March 2017

Wilaya za Mwanga na Same zajiunga iCHF

Hatimaye wilaya za Mwanga na Same zimejiunga rasmi na Mfuko wa Afya ya Jamii ulioboreshwa (iCHF), tayari kupata huduma bora zaidi kuliko ilivyokuwa chini ya Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).

Wilaya mbili hizo zimeingia iCHF baada ya nyingine mkoani Kilimanjaro za Siha, Hai, Moshi na Rombo. Madiwani wao wameidhinisha kujiunga huko baada ya kujiridhisha juu ya ubora wake.


Madiwani hao walipatiwa semina na maofisa wa shirika lisilo la kiserikali la PharmAccess International, akiwamo Prosper Msuya na Meneja wa Mkoa wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Fidelis Shauritanga.


Baada ya kupatiwa semina juu ya upungufu uliokuwapo kwenye CHF na faida zitakazopatikana kwenye iCHF, madiwani wa Mwanga na Same, kwa siku tofauti na kila kundi kwenye wilaya yao, waliitisha vikao vya Baraza la Madiwani.


Katika vikao hivyo, madiwani wa wilaya zote walitoa michango kwenye hoja husika na hatimaye kupitisha uamuzi kwa kauli moja kuridhia wilaya hizo kujiunga kwenye mpango huo mpya.

Madiwani waliridhia kwamba badala ya 10,000/- walizokuwa wakilipa wananchi wao chini ya CHF na kuminywa katika upana na kiwango cha huduma za afya, sasa walipe 30,000/- kwa familia ya watu sita kila mwaka.


Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani la Mwanga, Bibi Theresia Msuya aliwaasa madiwani wenzake kuingia kwenye maeneo yao, iwe kwenye mikutano ya hadhara au nyumba kwa nyumba, kuhamasisha wananchi ili wajiunge iCHF.


Bibi Msuya alisema mfuko huo wa afya ya jamii ulioboreshwa utawafaa sana wananchi ili waepuke mzigo wa gharama kubwa za huduma za afya.
Kadhalika alisema kiwango kilichowekwa kina mantiki.



Bibi Msuya aliwaomba madiwani kujitolea pia kulipiua fedha baadhi ya familia zisizojiweza, akisema anajua kwamba wapo wanaoweza kuchangia hata familia tatu, ikimaanisha 90,000/-


Madiwani walitoa mwito kwa wafanyakazi wa kwenye vituo  vya afya, zahanati na hospitali kuwa na lugha nzuri kwa wagonjwa lakini pia kuhakikisha wanatoa vyema huduma kwao.


Meneja wa NHIF Mkoa wa Kilimanjaro, Bw. Fidelis Shauritanga aliwapongeza madiwani wa Mwanga na Same kwa hatua yao ya kuidhinisha iCHF. Alisema mkoa sasa umekuwa wa kupigiwa mfano, lakini pia kioo kwa wengine ambao hufika kujifunza jinsi iCHF inavyofanya kazi. Alisema hata maofisa kutoka nchini Ethiopia walifika kwa ajili hiyo.

Meneja wa PharmAccess, Bw. Prosper Msuya alieleza wameondokana na CHF na kuingia iCHF kwa sababu CHF ilielemewa na majukumu, ikiwa na watumishi wachache na hapakuwa na namna ya udhibiti kuhakikisha huduma zinatolewa inavyotakiwa.

Bw. Msuya alisema pia kwamba hapakuwapo na kupata mrejesho juu ya kiwango cha huduma, lakini pia 10,000/- hakikuwa kiwango cha kukidhi gharama za watu sita kwa mwaka, hata kama wengine hawangeugua.


Ofisa huyo alisema kimsingi hiyo ya awali haikuendana na sera na miongozo ya bima, kwani wagonjwa ndio walioandikishwa hospitalini wakati bima hukatwa kabla ya tukio tarajiwa kutokea. Alitoa mfano wa bima za magari, ambapo huwezi kukatia bima gari na ukapata baada ya gari kupata ajali na kuharibika.


Chini ya iCHF, watakuwapo watu maalumu kwa ajili ya kuandikisha majumbani na kwenye vituo vitakavyopangwa, kila mwanachama atapata kadi yake, tofauti na ilivyokuwa chini ya CHF. Tayari mfumo huo umethibitishwa kuwa bora wilayani Siha, Hai, Moshi na Rombo.


Wateja wanne wategemezi na wazazi/walezi wawili watachagua vituo viwili vya huduma, kimoja cha awali na kingine cha rufaa na watakuwa na haki ya kuhamia vingine/kingine kila baada ya miezi mitatu.
Watapata huduma mbalimbali, ikiwa ni pamoja na upasuaji wa dharura, kama kujifungua na baada ya ajali.



 Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Bw. Aaron Mbogo aliwapongeza wadau kwa kuja na huduma hiyo mpya, akasema mtu akiwa na bima anakuwa na amani akilini mwake kwani anajua wakati wowote akiugua atapata huduma za afya zenye kiwango kikubwa. Aliahidi kushiriki kwenye kampeni kuhamasisha watu kujiunga na mfuko huo ulioboreshwa.