Sunday, 26 March 2017

Wanakijiji wanavyofaidika na CHF iliyoboreshwa

Wanakijiji wametoa ushuhuda juu ya kufaidika kwao na Mfuko wa Afya ya Jamii ulioboreshwa (iCHF).

Wanakijiji hao wa Singa, Kata ya Kibosho Mashariki, Tarafa ya Kibosho, Wilaya ya Moshi Vijijini wameelezea kufurahishwa na kupatiwa huduma za afya zenye kiwango cha juu bila usumbufu, tena kwa gharama nafuu.

Wilaya ya Moshi Vijijini ni miongoni mwa wilaya za Mkoa wa Kilimanjaro na Manyara zinazopata huduma ya iCHF. Nyingine mkoani Kilimanjaro ni Siha, Hai, Rombo, Mwanga na Same.

Mmoja wa wafaidika hao, Bw Faustine Leruba anasema kwamba CHF iliyoboreshwa imemsaidia sana na mke wake, kwa sababu sasa kila akihisi kuumwa huenda hospitalini na kupata matibabu na kwamba kwenye hii iliyoboreshwa hakuna usumbufu, na dawa hupatikana vizuri. Amekuwa akipata matibabu katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Kibosho.

Bw Leruba (72) alijiunga na iCHF Februari mwaka jana (2016) baada ya Wasamaria wema kumsaidia fedha kwa ajili hiyo, ambapo amejiunga pamoja na mkewe. Anasema kwa kujiunga huko, kwa kulipia 30,000/- kwa mwaka kunawapunguzia sana gharama kubwa za matibabu. Anakiri kwamba hakuwa akiujua mpango huo hadi aliposikia ukitangazwa kwenye Ibada ya Misa Jumapili katika Kanisa Katoliki Kibosho, karibu kabisa na Kibosho Hospitali.

Hata hivyo, Leruba anasema kwamba hakuweza kujiunga kwani aliona kwamba hakuwa na fedha, japokuwa akiugua angefanya kila awezalo kupata fedha kwa ajili ya matibabu na wakati mwingine angekopa kwa marafiki au majirani. Anasema kwamba kwa wastani kila akienda hospitali kwa ajili ya matibabu aliingia gharama ya zaidi ya 10,000/-.

Akifafanua zaidi juu ya hali hiyo, anasema ukokotozi unaonesha kwamba malipo yaliyofanywa na familia yake kwa ajili ya matibabu kwa mwaka ni zaidi ya 300,000/- ikiwa hawatumii iCHF, kwani huenda hospitali mara kwa mara kwa sababu ana matatizo ya miguu – gauti.
Anasema kwamba mbali ya yeye kuugua na kuhitaji matibabu mara kwa mara, mkewe pia ana matatizo makubwa ya kifua, hivyo hutakiwa kwenda hospitali mara kwa mara kwa ajili ya uangalizi na matibabu. Anasema laiti wasingekuwa na CHF iliyoboreshwa, basi wangedidimia zaidi kwenye umasikini. Bw Leruba alikuwa muuza duka jijini Dar es Salaam kwa miaka mingi kabla ya kuamua kurejea kijijini baada ya maisha kumpiga kwenye jiji hilo kuu kibiashara. Mkewe ni mfanyabiashara, anayetengeneza na kuuza pombe ya mbege kwa jumla.

iCHF sasa inatekelezwa na mabaraza ya halmashauri za wilaya chini ya ulezi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF). Shirika lisilo la kiserikali – PharmAccess hutoa usaidizi wa kiufundi kwa ajili ya utawala na kuboresha huduma za afya pamoja na shughuli za masoko kwa ajili ya iCHF.

Ili kuboresha kiwango cha huduma za afya, zahanati, vituo vya afya na hospitali za umma na binafsi zilizo kwenye iCHF zimeingizwa kwenye program ya SafeCare. NHIF na PharmAccess kwa pamoja huwezesha uboreshaji wa miundombinu kwenye huduma zinakotolewa, kwa kuvutia uwekezaji, kuhakikisha huduma bora zinatolewa na mpango huu na kijiografia kuongeza maeneo yanayopatiwa huduma.

Mlengwa mwingine ni Bw Dionis Neneu (67), kutoka kijiji hicho hicho, anayesema kwamba anafurahia huduma ya kiwango kizuri ya afya bila kuingia kwenye tabu ya kutafuta fedha kila mara kwa ajili ya kugharamia, huku akiwa hajui ingegharimu kiasi gani cha fedha.

Bw Neneu anasema kwamba alihuisha huduma hiyo ya CHF iliyoboreshwa Januari mwaka huu, kwani kwa mara ya kwanza alikatiwa na mtoto wake mwaka jana, ambapo iCHF hiyo inamhusu yeye na mkewe.

Wanafurahia maisha kwa sabbau katika umri wao mkubwa wanapata huduma ya afya kila wakati wanapoihitaji. Wote wawili ni wakulima ambao pia hufuga ng’ombe nyumbani kwao.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Singa, Bw Paul Lazaro anasema pamekuwa na mwamko mkubwa wa watu wanaojitokeza kwa ajili ya kujiunga iCHF. Hali hiyo, anasema, inatokana na watu kuongezewa uelewa juu ya umuhimu wa kuwa na bima, kazi ambayo imekuwa ikifanywa na maofisa au wadau wa NHIF kwenye nyumba za ibada na viongozi wa kisiasa kwenye mikutano mtawalia.

Chini ya mpango huo, kaya inaweza kuorodhesha hadi wana familia sita hivyo kuwa na haki ya kupatiwa huduma za matibabu n ahata kulazwa hata kwa magonjwa makubwa, huduma ya msingi ya meno pamoja na upasuaji wa dharura, ukihusisha pia wakati wa uzazi. Serikali, kupitia NHIF, hujazia asilimia 50 ya gharama kwa kundi husika.


Ile hali ya kufanya wananchi wamiliki mpango wenyewe, huku kukiwapo na kujengewa uwezo kutoka kwa PharmAccess, husaidia na kuhakikisha kwamba unakuwa mradi endelevu.

No comments:

Post a Comment