Hatimaye wilaya za Mwanga na Same
zimejiunga rasmi na Mfuko wa Afya ya Jamii ulioboreshwa (iCHF), tayari kupata
huduma bora zaidi kuliko ilivyokuwa chini ya Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).
Wilaya mbili hizo zimeingia iCHF baada
ya nyingine mkoani Kilimanjaro za Siha, Hai, Moshi na Rombo. Madiwani wao
wameidhinisha kujiunga huko baada ya kujiridhisha juu ya ubora wake.
Madiwani hao walipatiwa semina na
maofisa wa shirika lisilo la kiserikali la PharmAccess International, akiwamo
Prosper Msuya na Meneja wa Mkoa wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF),
Fidelis Shauritanga.
Baada ya kupatiwa semina juu ya upungufu
uliokuwapo kwenye CHF na faida zitakazopatikana kwenye iCHF, madiwani wa Mwanga
na Same, kwa siku tofauti na kila kundi kwenye wilaya yao, waliitisha vikao vya
Baraza la Madiwani.
Katika vikao hivyo, madiwani wa wilaya
zote walitoa michango kwenye hoja husika na hatimaye kupitisha uamuzi kwa kauli
moja kuridhia wilaya hizo kujiunga kwenye mpango huo mpya.
Madiwani waliridhia kwamba badala ya
10,000/- walizokuwa wakilipa wananchi wao chini ya CHF na kuminywa katika upana
na kiwango cha huduma za afya, sasa walipe 30,000/- kwa familia ya watu sita
kila mwaka.
Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani la
Mwanga, Bibi Theresia Msuya aliwaasa madiwani wenzake kuingia kwenye maeneo
yao, iwe kwenye mikutano ya hadhara au nyumba kwa nyumba, kuhamasisha wananchi
ili wajiunge iCHF.
Bibi Msuya alisema mfuko huo wa afya ya
jamii ulioboreshwa utawafaa sana wananchi ili waepuke mzigo wa gharama kubwa za
huduma za afya.
Kadhalika alisema kiwango kilichowekwa
kina mantiki.
Bibi Msuya aliwaomba madiwani kujitolea
pia kulipiua fedha baadhi ya familia zisizojiweza, akisema anajua kwamba wapo
wanaoweza kuchangia hata familia tatu, ikimaanisha 90,000/-
Madiwani walitoa mwito kwa wafanyakazi
wa kwenye vituo vya afya, zahanati na
hospitali kuwa na lugha nzuri kwa wagonjwa lakini pia kuhakikisha wanatoa vyema
huduma kwao.
Meneja wa NHIF Mkoa wa Kilimanjaro, Bw.
Fidelis Shauritanga aliwapongeza madiwani wa Mwanga na Same kwa hatua yao ya
kuidhinisha iCHF. Alisema mkoa sasa umekuwa wa kupigiwa mfano, lakini pia kioo
kwa wengine ambao hufika kujifunza jinsi iCHF inavyofanya kazi. Alisema hata
maofisa kutoka nchini Ethiopia walifika kwa ajili hiyo.
Meneja wa PharmAccess, Bw. Prosper Msuya
alieleza wameondokana na CHF na kuingia iCHF kwa sababu CHF ilielemewa na
majukumu, ikiwa na watumishi wachache na hapakuwa na namna ya udhibiti
kuhakikisha huduma zinatolewa inavyotakiwa.
Bw. Msuya alisema pia kwamba hapakuwapo
na kupata mrejesho juu ya kiwango cha huduma, lakini pia 10,000/- hakikuwa
kiwango cha kukidhi gharama za watu sita kwa mwaka, hata kama wengine
hawangeugua.
Ofisa huyo alisema kimsingi hiyo ya
awali haikuendana na sera na miongozo ya bima, kwani wagonjwa ndio
walioandikishwa hospitalini wakati bima hukatwa kabla ya tukio tarajiwa
kutokea. Alitoa mfano wa bima za magari, ambapo huwezi kukatia bima gari na ukapata
baada ya gari kupata ajali na kuharibika.
Chini ya iCHF, watakuwapo watu maalumu
kwa ajili ya kuandikisha majumbani na kwenye vituo vitakavyopangwa, kila
mwanachama atapata kadi yake, tofauti na ilivyokuwa chini ya CHF. Tayari mfumo
huo umethibitishwa kuwa bora wilayani Siha, Hai, Moshi na Rombo.
Wateja wanne wategemezi na wazazi/walezi
wawili watachagua vituo viwili vya huduma, kimoja cha awali na kingine cha
rufaa na watakuwa na haki ya kuhamia vingine/kingine kila baada ya miezi
mitatu.
Watapata huduma mbalimbali, ikiwa ni
pamoja na upasuaji wa dharura, kama kujifungua na baada ya ajali.
Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Bw. Aaron Mbogo
aliwapongeza wadau kwa kuja na huduma hiyo mpya, akasema mtu akiwa na bima
anakuwa na amani akilini mwake kwani anajua wakati wowote akiugua atapata
huduma za afya zenye kiwango kikubwa. Aliahidi kushiriki kwenye kampeni
kuhamasisha watu kujiunga na mfuko huo ulioboreshwa.
No comments:
Post a Comment