Wanakijiji wametoa ushuhuda juu ya
kufaidika kwao na Mfuko wa Afya ya Jamii ulioboreshwa (iCHF).
Wanakijiji hao wa Singa, Kata ya Kibosho
Mashariki, Tarafa ya Kibosho, Wilaya ya Moshi Vijijini wameelezea kufurahishwa
na kupatiwa huduma za afya zenye kiwango cha juu bila usumbufu, tena kwa
gharama nafuu.
Wilaya ya Moshi Vijijini ni miongoni mwa
wilaya za Mkoa wa Kilimanjaro na Manyara zinazopata huduma ya iCHF. Nyingine
mkoani Kilimanjaro ni Siha, Hai, Rombo, Mwanga na Same.
Mmoja wa wafaidika hao, Bw Faustine Leruba
anasema kwamba CHF iliyoboreshwa imemsaidia sana na mke wake, kwa sababu sasa
kila akihisi kuumwa huenda hospitalini na kupata matibabu na kwamba kwenye hii
iliyoboreshwa hakuna usumbufu, na dawa hupatikana vizuri. Amekuwa akipata
matibabu katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Kibosho.
Bw Leruba (72) alijiunga na iCHF Februari
mwaka jana (2016) baada ya Wasamaria wema kumsaidia fedha kwa ajili hiyo,
ambapo amejiunga pamoja na mkewe. Anasema kwa kujiunga huko, kwa kulipia
30,000/- kwa mwaka kunawapunguzia sana gharama kubwa za matibabu. Anakiri
kwamba hakuwa akiujua mpango huo hadi aliposikia ukitangazwa kwenye Ibada ya
Misa Jumapili katika Kanisa Katoliki Kibosho, karibu kabisa na Kibosho
Hospitali.
Hata hivyo, Leruba anasema kwamba hakuweza
kujiunga kwani aliona kwamba hakuwa na fedha, japokuwa akiugua angefanya kila
awezalo kupata fedha kwa ajili ya matibabu na wakati mwingine angekopa kwa
marafiki au majirani. Anasema kwamba kwa wastani kila akienda hospitali kwa
ajili ya matibabu aliingia gharama ya zaidi ya 10,000/-.
Akifafanua zaidi juu ya hali hiyo, anasema
ukokotozi unaonesha kwamba malipo yaliyofanywa na familia yake kwa ajili ya
matibabu kwa mwaka ni zaidi ya 300,000/- ikiwa hawatumii iCHF, kwani huenda
hospitali mara kwa mara kwa sababu ana matatizo ya miguu – gauti.
Anasema kwamba mbali ya yeye kuugua na
kuhitaji matibabu mara kwa mara, mkewe pia ana matatizo makubwa ya kifua, hivyo
hutakiwa kwenda hospitali mara kwa mara kwa ajili ya uangalizi na matibabu.
Anasema laiti wasingekuwa na CHF iliyoboreshwa, basi wangedidimia zaidi kwenye
umasikini. Bw Leruba alikuwa muuza duka jijini Dar es Salaam kwa miaka mingi
kabla ya kuamua kurejea kijijini baada ya maisha kumpiga kwenye jiji hilo kuu
kibiashara. Mkewe ni mfanyabiashara, anayetengeneza na kuuza pombe ya mbege kwa
jumla.
iCHF sasa inatekelezwa na mabaraza ya
halmashauri za wilaya chini ya ulezi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Shirika lisilo la kiserikali – PharmAccess hutoa usaidizi wa kiufundi kwa ajili
ya utawala na kuboresha huduma za afya pamoja na shughuli za masoko kwa ajili
ya iCHF.
Ili kuboresha kiwango cha huduma za afya,
zahanati, vituo vya afya na hospitali za umma na binafsi zilizo kwenye iCHF
zimeingizwa kwenye program ya SafeCare. NHIF na PharmAccess kwa pamoja
huwezesha uboreshaji wa miundombinu kwenye huduma zinakotolewa, kwa kuvutia
uwekezaji, kuhakikisha huduma bora zinatolewa na mpango huu na kijiografia
kuongeza maeneo yanayopatiwa huduma.
Mlengwa mwingine ni Bw Dionis Neneu (67),
kutoka kijiji hicho hicho, anayesema kwamba anafurahia huduma ya kiwango kizuri
ya afya bila kuingia kwenye tabu ya kutafuta fedha kila mara kwa ajili ya
kugharamia, huku akiwa hajui ingegharimu kiasi gani cha fedha.
Bw Neneu anasema kwamba alihuisha huduma
hiyo ya CHF iliyoboreshwa Januari mwaka huu, kwani kwa mara ya kwanza alikatiwa
na mtoto wake mwaka jana, ambapo iCHF hiyo inamhusu yeye na mkewe.
Wanafurahia maisha kwa sabbau katika umri
wao mkubwa wanapata huduma ya afya kila wakati wanapoihitaji. Wote wawili ni
wakulima ambao pia hufuga ng’ombe nyumbani kwao.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Singa, Bw Paul
Lazaro anasema pamekuwa na mwamko mkubwa wa watu wanaojitokeza kwa ajili ya
kujiunga iCHF. Hali hiyo, anasema, inatokana na watu kuongezewa uelewa juu ya
umuhimu wa kuwa na bima, kazi ambayo imekuwa ikifanywa na maofisa au wadau wa
NHIF kwenye nyumba za ibada na viongozi wa kisiasa kwenye mikutano mtawalia.
Chini ya mpango huo, kaya inaweza
kuorodhesha hadi wana familia sita hivyo kuwa na haki ya kupatiwa huduma za
matibabu n ahata kulazwa hata kwa magonjwa makubwa, huduma ya msingi ya meno
pamoja na upasuaji wa dharura, ukihusisha pia wakati wa uzazi. Serikali,
kupitia NHIF, hujazia asilimia 50 ya gharama kwa kundi husika.
Ile hali ya kufanya wananchi wamiliki
mpango wenyewe, huku kukiwapo na kujengewa uwezo kutoka kwa PharmAccess,
husaidia na kuhakikisha kwamba unakuwa mradi endelevu.