Friday, 16 June 2017
Mkutano wa wadau wa iCHF - Kilimanjaro
Wenyeviti wa Halmashauri za Kilimanjaro, Wakurugenzi wa halmashauri na wadau wengine wakihudhuria mkutano wa nusu mwaka wa wadau wa iCHF
Monday, 29 May 2017
Mwanga na Same, tumewafikia......
Kaimu Mkurugenzi halmashauri ya same (Juu) akijaribu pikipiki kabla hajaikabidhi kwa waratibu wa CHF iliyoboreshwa wa tarafa. Chini, Mkurugenzi wa halmashauri ya Mwanga akimkabidhi pikipiki mmoja ya mratibu wa tarafa tayari kwa kuanza kazi ya usajili CHF iliyoboreshwa
Sunday, 26 March 2017
Wanakijiji wanavyofaidika na CHF iliyoboreshwa
Wanakijiji wametoa ushuhuda juu ya
kufaidika kwao na Mfuko wa Afya ya Jamii ulioboreshwa (iCHF).
Wanakijiji hao wa Singa, Kata ya Kibosho
Mashariki, Tarafa ya Kibosho, Wilaya ya Moshi Vijijini wameelezea kufurahishwa
na kupatiwa huduma za afya zenye kiwango cha juu bila usumbufu, tena kwa
gharama nafuu.
Wilaya ya Moshi Vijijini ni miongoni mwa
wilaya za Mkoa wa Kilimanjaro na Manyara zinazopata huduma ya iCHF. Nyingine
mkoani Kilimanjaro ni Siha, Hai, Rombo, Mwanga na Same.
Mmoja wa wafaidika hao, Bw Faustine Leruba
anasema kwamba CHF iliyoboreshwa imemsaidia sana na mke wake, kwa sababu sasa
kila akihisi kuumwa huenda hospitalini na kupata matibabu na kwamba kwenye hii
iliyoboreshwa hakuna usumbufu, na dawa hupatikana vizuri. Amekuwa akipata
matibabu katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Kibosho.
Bw Leruba (72) alijiunga na iCHF Februari
mwaka jana (2016) baada ya Wasamaria wema kumsaidia fedha kwa ajili hiyo,
ambapo amejiunga pamoja na mkewe. Anasema kwa kujiunga huko, kwa kulipia
30,000/- kwa mwaka kunawapunguzia sana gharama kubwa za matibabu. Anakiri
kwamba hakuwa akiujua mpango huo hadi aliposikia ukitangazwa kwenye Ibada ya
Misa Jumapili katika Kanisa Katoliki Kibosho, karibu kabisa na Kibosho
Hospitali.
Hata hivyo, Leruba anasema kwamba hakuweza
kujiunga kwani aliona kwamba hakuwa na fedha, japokuwa akiugua angefanya kila
awezalo kupata fedha kwa ajili ya matibabu na wakati mwingine angekopa kwa
marafiki au majirani. Anasema kwamba kwa wastani kila akienda hospitali kwa
ajili ya matibabu aliingia gharama ya zaidi ya 10,000/-.
Akifafanua zaidi juu ya hali hiyo, anasema
ukokotozi unaonesha kwamba malipo yaliyofanywa na familia yake kwa ajili ya
matibabu kwa mwaka ni zaidi ya 300,000/- ikiwa hawatumii iCHF, kwani huenda
hospitali mara kwa mara kwa sababu ana matatizo ya miguu – gauti.
Anasema kwamba mbali ya yeye kuugua na
kuhitaji matibabu mara kwa mara, mkewe pia ana matatizo makubwa ya kifua, hivyo
hutakiwa kwenda hospitali mara kwa mara kwa ajili ya uangalizi na matibabu.
Anasema laiti wasingekuwa na CHF iliyoboreshwa, basi wangedidimia zaidi kwenye
umasikini. Bw Leruba alikuwa muuza duka jijini Dar es Salaam kwa miaka mingi
kabla ya kuamua kurejea kijijini baada ya maisha kumpiga kwenye jiji hilo kuu
kibiashara. Mkewe ni mfanyabiashara, anayetengeneza na kuuza pombe ya mbege kwa
jumla.
iCHF sasa inatekelezwa na mabaraza ya
halmashauri za wilaya chini ya ulezi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Shirika lisilo la kiserikali – PharmAccess hutoa usaidizi wa kiufundi kwa ajili
ya utawala na kuboresha huduma za afya pamoja na shughuli za masoko kwa ajili
ya iCHF.
Ili kuboresha kiwango cha huduma za afya,
zahanati, vituo vya afya na hospitali za umma na binafsi zilizo kwenye iCHF
zimeingizwa kwenye program ya SafeCare. NHIF na PharmAccess kwa pamoja
huwezesha uboreshaji wa miundombinu kwenye huduma zinakotolewa, kwa kuvutia
uwekezaji, kuhakikisha huduma bora zinatolewa na mpango huu na kijiografia
kuongeza maeneo yanayopatiwa huduma.
Mlengwa mwingine ni Bw Dionis Neneu (67),
kutoka kijiji hicho hicho, anayesema kwamba anafurahia huduma ya kiwango kizuri
ya afya bila kuingia kwenye tabu ya kutafuta fedha kila mara kwa ajili ya
kugharamia, huku akiwa hajui ingegharimu kiasi gani cha fedha.
Bw Neneu anasema kwamba alihuisha huduma
hiyo ya CHF iliyoboreshwa Januari mwaka huu, kwani kwa mara ya kwanza alikatiwa
na mtoto wake mwaka jana, ambapo iCHF hiyo inamhusu yeye na mkewe.
Wanafurahia maisha kwa sabbau katika umri
wao mkubwa wanapata huduma ya afya kila wakati wanapoihitaji. Wote wawili ni
wakulima ambao pia hufuga ng’ombe nyumbani kwao.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Singa, Bw Paul
Lazaro anasema pamekuwa na mwamko mkubwa wa watu wanaojitokeza kwa ajili ya
kujiunga iCHF. Hali hiyo, anasema, inatokana na watu kuongezewa uelewa juu ya
umuhimu wa kuwa na bima, kazi ambayo imekuwa ikifanywa na maofisa au wadau wa
NHIF kwenye nyumba za ibada na viongozi wa kisiasa kwenye mikutano mtawalia.
Chini ya mpango huo, kaya inaweza
kuorodhesha hadi wana familia sita hivyo kuwa na haki ya kupatiwa huduma za
matibabu n ahata kulazwa hata kwa magonjwa makubwa, huduma ya msingi ya meno
pamoja na upasuaji wa dharura, ukihusisha pia wakati wa uzazi. Serikali,
kupitia NHIF, hujazia asilimia 50 ya gharama kwa kundi husika.
Ile hali ya kufanya wananchi wamiliki
mpango wenyewe, huku kukiwapo na kujengewa uwezo kutoka kwa PharmAccess,
husaidia na kuhakikisha kwamba unakuwa mradi endelevu.
Saturday, 4 March 2017
Friday, 3 March 2017
Uboreshaji wa huduma unaofanywa na iCHF
Ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora, iCHF imekuwa ikisaidia uboreshaji wa huduma kwenye zahanati na vituo vya afya wilayani.
Madiwani Mwanga, Same wapitisha CHF iliyoboreshwa kuanza wilayani kwao!
Waheshimiwa madiwani wa halmashauri ya Mwanga wakimsikiliza meneja wa mkoa wa Kilimanjaro wakati wa semina kwa madiwani kuhusu CHF iliyoboreshwa.
Thursday, 2 March 2017
Wilaya za Mwanga na Same zajiunga iCHF
Hatimaye wilaya za Mwanga na Same
zimejiunga rasmi na Mfuko wa Afya ya Jamii ulioboreshwa (iCHF), tayari kupata
huduma bora zaidi kuliko ilivyokuwa chini ya Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).
Wilaya mbili hizo zimeingia iCHF baada
ya nyingine mkoani Kilimanjaro za Siha, Hai, Moshi na Rombo. Madiwani wao
wameidhinisha kujiunga huko baada ya kujiridhisha juu ya ubora wake.
Madiwani hao walipatiwa semina na
maofisa wa shirika lisilo la kiserikali la PharmAccess International, akiwamo
Prosper Msuya na Meneja wa Mkoa wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF),
Fidelis Shauritanga.
Baada ya kupatiwa semina juu ya upungufu
uliokuwapo kwenye CHF na faida zitakazopatikana kwenye iCHF, madiwani wa Mwanga
na Same, kwa siku tofauti na kila kundi kwenye wilaya yao, waliitisha vikao vya
Baraza la Madiwani.
Katika vikao hivyo, madiwani wa wilaya
zote walitoa michango kwenye hoja husika na hatimaye kupitisha uamuzi kwa kauli
moja kuridhia wilaya hizo kujiunga kwenye mpango huo mpya.
Madiwani waliridhia kwamba badala ya
10,000/- walizokuwa wakilipa wananchi wao chini ya CHF na kuminywa katika upana
na kiwango cha huduma za afya, sasa walipe 30,000/- kwa familia ya watu sita
kila mwaka.
Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani la
Mwanga, Bibi Theresia Msuya aliwaasa madiwani wenzake kuingia kwenye maeneo
yao, iwe kwenye mikutano ya hadhara au nyumba kwa nyumba, kuhamasisha wananchi
ili wajiunge iCHF.
Bibi Msuya alisema mfuko huo wa afya ya
jamii ulioboreshwa utawafaa sana wananchi ili waepuke mzigo wa gharama kubwa za
huduma za afya.
Kadhalika alisema kiwango kilichowekwa
kina mantiki.
Bibi Msuya aliwaomba madiwani kujitolea
pia kulipiua fedha baadhi ya familia zisizojiweza, akisema anajua kwamba wapo
wanaoweza kuchangia hata familia tatu, ikimaanisha 90,000/-
Madiwani walitoa mwito kwa wafanyakazi
wa kwenye vituo vya afya, zahanati na
hospitali kuwa na lugha nzuri kwa wagonjwa lakini pia kuhakikisha wanatoa vyema
huduma kwao.
Meneja wa NHIF Mkoa wa Kilimanjaro, Bw.
Fidelis Shauritanga aliwapongeza madiwani wa Mwanga na Same kwa hatua yao ya
kuidhinisha iCHF. Alisema mkoa sasa umekuwa wa kupigiwa mfano, lakini pia kioo
kwa wengine ambao hufika kujifunza jinsi iCHF inavyofanya kazi. Alisema hata
maofisa kutoka nchini Ethiopia walifika kwa ajili hiyo.
Meneja wa PharmAccess, Bw. Prosper Msuya
alieleza wameondokana na CHF na kuingia iCHF kwa sababu CHF ilielemewa na
majukumu, ikiwa na watumishi wachache na hapakuwa na namna ya udhibiti
kuhakikisha huduma zinatolewa inavyotakiwa.
Bw. Msuya alisema pia kwamba hapakuwapo
na kupata mrejesho juu ya kiwango cha huduma, lakini pia 10,000/- hakikuwa
kiwango cha kukidhi gharama za watu sita kwa mwaka, hata kama wengine
hawangeugua.
Ofisa huyo alisema kimsingi hiyo ya
awali haikuendana na sera na miongozo ya bima, kwani wagonjwa ndio
walioandikishwa hospitalini wakati bima hukatwa kabla ya tukio tarajiwa
kutokea. Alitoa mfano wa bima za magari, ambapo huwezi kukatia bima gari na ukapata
baada ya gari kupata ajali na kuharibika.
Chini ya iCHF, watakuwapo watu maalumu
kwa ajili ya kuandikisha majumbani na kwenye vituo vitakavyopangwa, kila
mwanachama atapata kadi yake, tofauti na ilivyokuwa chini ya CHF. Tayari mfumo
huo umethibitishwa kuwa bora wilayani Siha, Hai, Moshi na Rombo.
Wateja wanne wategemezi na wazazi/walezi
wawili watachagua vituo viwili vya huduma, kimoja cha awali na kingine cha
rufaa na watakuwa na haki ya kuhamia vingine/kingine kila baada ya miezi
mitatu.
Watapata huduma mbalimbali, ikiwa ni
pamoja na upasuaji wa dharura, kama kujifungua na baada ya ajali.
Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Bw. Aaron Mbogo
aliwapongeza wadau kwa kuja na huduma hiyo mpya, akasema mtu akiwa na bima
anakuwa na amani akilini mwake kwani anajua wakati wowote akiugua atapata
huduma za afya zenye kiwango kikubwa. Aliahidi kushiriki kwenye kampeni
kuhamasisha watu kujiunga na mfuko huo ulioboreshwa.
Monday, 20 February 2017
Wakina mama ndio wakutukomboa kwenye masuala ya Afya!
Kitenge humuweka salama mtoto mgongoni kwa mama yake. Kwa gharama sawa na ya kununua kitenge unaweza kuilipia familia yako nzima bima ya afya ya iCHF kuwakinga afya zao. JE! ni kwanini wakina mama wengi hawana mwamko wa kulipia bima ya afya wakati inafahamika wao na watoto ndio watumiaji wakubwa wa huduma za afya?
Sunday, 19 February 2017
Wananchi 172,115 wanaendelea kunufaika Kilimanjaro na Manyara
Mpaka December 2016, Jumla ya wakazi 172,115 wa mikoa ya Kilimanjaro na Manyara wameendelea kunufaika na huduma ya CHF iliyoboreshwa katika hospitali za binafsi na zile za serikali. Na wewe unaweza kujiunga nao au kulipia ndugu zako walioko huko. Pia kuna nyumba za watoto yatima unaweza kuwalipia, elfu (Yatima watano watalipiwa elfu 30,000 kwa mwaka mzima)
Wednesday, 25 January 2017
Tupe maoni yako!
Juhudi kubwa zinafanyika na serikali na wadau kuhakikisha wananchi wote wanajiunga na bima ya afya, ili waweze kupata huduma bora za afya wakati wote wanaozihitaji. Mfano mzuri ni iCHF, ambako unalipa elfu thelasini (30,000) tu na familia nzima mnatibiwa mwaka mzima bila malipo, ikiwemo na huduma za kulazwa na hata upasuaji wa dharula.JE, UNADHANI KWA NINI WATU HAWATAKI KUJIUNGA KATIKA MIFUKO YA BIMA ZA AFYA?
Subscribe to:
Posts (Atom)